Posted on: December 6, 2019 Posted by: Kamadi Amata Comments: 0

Gavana wa Nairobi Mike Sonko alikamatwa na makachero wa tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC eneo la Voi. Haya yalijiri saa chache baada ya kiongozi wa mashtaka ya umma Noordin Haji kuamrisha kukamatwa kwa Gavana huyo akisema kuwa uchunguzi waliofanya unamhusisha na ubadhirifu wa shilingi milioni 357.

Mzozo uliibuka kati ya Gavana huyo na maafisa wa polisi barabarani baada ya kudaiwa Gavana huyo alidinda kupanda helikopta ya polisi. Hatimaye alilazimishwa na kupelekwa katika afisi za EACC jijini Nairobi kuandikisha taarifa akingoja kushtakiwa mahakamani.

Noordin Haji pia akihutubia wanahabari, alitoa wito kwa idara ya mahakama kuhakikisha mkondo wa sheria umefuatwa kwa kesi zinazohusu ufisadi. Iwapo Gavana atashtakiwa mahakamani, atalazimika kun’gatuka mamlakani kwa muda huku uchunguzi ukiendelea na kupisha spika wa kaunti Beatrice Elachi kushikilia nafasi hiyo kwani hakuwa ameteua Naibu Gavana.