Wakenya wanaoishi mijini wameshauriwa wasisafiri kuelekea mashinani wakati huu ambapo serikali inajitahidi iwezavyo kudhibiti ueneaji wa virusi vya corona. Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliffe Oparanya, alisema kuhepa mijini itawaweka wakazi hao pamoja na jamaa zao katika hatari ya kuambukizwa virusi hivyo hatari.
Oparanya pia anahofia kwamba, kuna wazee wengi wanaoishi vijijini, na wazee wametambuliwa kuwa katika hatari zaidi ya kupata madhara makubwa endapo wataambukizwa. Kiongozi huyo ambaye pia ni Gavana wa Kakamega aliongezea kuwa njia bora ya kujikinga na virusi hivyo ni kuosha mikono kwa sabuni kila mara na kuepuka maeneo yaliyo na watu wengi.
Hii ni baada ya kuripotiwa kuwa wakazi wengi wa mijini hususan Nairobi wameanza kusafiri kwenda mashambani tangu kisa cha kwanza cha virusi vya corona kilipotangazwa nchini Ijumaa wiki iliyopita.