Waziri wa Fedha Ukur Yattani amekutana na viongozi wa seneti hivi leo.Mkutano ambao ulihudhuriwa na Spika wa seneti Ken Lusaka,kiongozi wa wengi kwenye seneti Samuel Poghisio,mwenyekiti wa baraza la magavana Wycliff Oparanya,msimamizi wa bajeti Margaret Nyakang’o na mkuu wa sheria Kihara Kariuki,wakiwemo wengine,wamezungumzia ugamvi wa fedha,2020.Haya yanajiri wiki moja baada ya maseneta kukosa kupitisha mgao wa fedha kwenye seneti.
Mfumo huo tatanishi unaonuia kutumia idadi ya watu kwa ugamvi wa fedha huenda ikaathiri kaunti zilizoachwa nyuma kimaendeleo kama kaunti za pwani,kaunti za kaskazini mashariki na baadhi ya maeneo ya magharibi.Maseneta kutoka maeneo haya walipinga mswada huu.
Wikendi hii,kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ambaye alikuwa akipata pingamizi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Jubilee,alikutana na Peter Kenneth,naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe,James Orengo na viongozi wengine katika makazi ya Francis Atwoli huko Kajiado ili kupata suluhisho.Mswada huu utawasilishwa kwa seneti jumatano hii.
Mwandishi: Ivy Otieno